Mambo 10 yatakayompagawisha
mwenziwako
1. WIVU
WA KUPINDUKIA.
Ni jambo jema kwa mwanamume
kumtakia heri mpenzi wake na kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa hapati
madhara, lakini iwapo utakuwa mtu wa wasiwasi na mashaka pale unapomwona mpenzi
wako akizungumza na mwanamume mwingine, au anapotoka na marafiki zake wa kike,
au anapovaa nguo inayomfanya atamanishe, basi fahamu kuwa tayari umekunywa sumu
ya mapenzi.
Katika uhusiano wa
kimapenzi, kuaminiana ni jambo muhimu sana. Kama kweli unataka mpenzi wako akupende
kwa dhati, mwoneshe kuwa unamwamini na unaheshimu maamuzi yake, ikiwa ni pamoja
na maamuzi ya kutoka na marafiki zake wa kike na kuwa na marafiki wa kawaida wa
kiume hivyo yakupasa kuondoa hofu na uachane kabisa kwa sababu wapo wanaume
ambao hutumia muda wao mwingi kuwapeleleza wapenzi wao ikiwa ni pamoja na
kuwategeshea kamera na rekoda za simu.
2. KUTOMWACHIA
NAFASI MPENZI
Kama huishi na mpenzi wako
ni jambo la kawaida kuwa na hamu ya kumwona mara kwa mara, lakini kumbuka kuwa
mpenzi wako naye ana maisha yake na anahitaji nafasi ya kuwa peke yake kwa
ajili ya mambo yake binafsi.
Hisia za kutaka kuwa na
mpenzi wako muda wote zinaweza kudhaniwa kuwa ni za mapenzi ya dhati, lakini
kwa hakika hiyo si ishara njema ya mapenzi ya kudumu.
Kwanza jiulize kama unaweza
kuendeleza hali hiyo maisha yako yote ni wazi kuwa utachoka, Kwa hiyo, mpe
mpenzi wako fursa ya kupumua, Namna hii mpenzi wako atajenga hamu ya kutaka
kukutana nawe lakini ukiwa naye muda wote hamu hiyo itaisha.
3. KUMWAMULIA
MPENZI MAMBO YAKE.
Unaweza kujikuta ukisukumwa
kumwambia mpenzi wako awe anavaa nini wakati gani, akutane na nani na kwa
wakati gani au ale nini. Ukiona hivyo, fahamu kuwa hayo si mapenzi, bali
umepitiliza na pengine mwisho wa uhusiano wenu unanukia.
Hata ukiachilia mbali suala
zima la usawa wa jinsia, hakuna mwanamke ambaye angependa apangiwe kila kitu
kuhusiana na maisha yake. Kama ilivyodokezwa hapo juu, kila mtu ana maisha yake
na kilichowaunganisha ni mapenzi tu. Kama utataka kumpangia kila kitu ni wazi
kuwa utaishia kuishi peke yako.
4. KUMUULIZA
MPENZI MASWALI.
Iwapo utajikuta ukimuuliza
mpenzi wako maswali mengi yanayoonesha wasiwasi wako kuhusiana na mwenendo
wake, fahamu kuwa kuna tatizo na tatizo hilo lisipopatiwa ufumbuzi utakuwa
mwanzo wa mwisho wa uhusiano wenu.
Mwanamke angependa umuulize
maswali ya kawaida kuhusiana na jinsi siku yake ilivyokuwa na kama marafiki
zake hawajambo au la, lakini kila jambo lina mpaka wake. Mwanamke hatarajii
kuwa kila mnapokutana atakuwa kama ameingia kwenye chumba cha mtihani au usaili
wa kazi.
5. KUTOAMINI
ANACHOKWELEZA MPENZI.
Wakati mwingine watu
hushindwa kuwaamini wenzao, lakini kwa sababu ambazo ni za msingi, lakini kuna
wakati ambapo mtu hushindwa kumwamini mwenzake bila sababu yoyote ya msingi, au
kwa sababu zisizo sahihi, kisingizio kikiwa ni mapenzi.
Kuna tatizo la kisaikolojia
la kujishuku au kuwashuku wenzako. Hili ni jambo ambalo linaweza kukuharibia
mustakabali wako katika mapenzi, maana husababisha kujengeka kwa mazingira ya
kutokuaminiana.
Ili uweze kwenda sanjari na
mpenzi wako, amini kila anachokweleza hadi pale utakapokuwa na sababu za msingi
za kutokumwamini. Na hata unapokuwa umelithibitisha jambo, endelea kuwa katika
uhalisia wako.
6. KUACHA
HOBI, MARAFIKI.
Mahusiano ya kimapenzi mara nyingi huhusisha kila mmoja
kuacha baadhi ya mambo yake kwa ajili ya mwenzake. Hata hivyo, lengo ni kuweka
tu uwiano wa mahitaji, si kuacha kila kitu ulichokuwa nacho kwa ajili ya
mwenzako, ama kwa shinikizo, au kwa kulewa penzi.
Iwapo utabaini kuwa marafiki
zako sasa wamekuwa ni marafiki zako wa zamani na hobi zako zimebaki tu katika
kumbukumbu japo kwa hakika bado unahisi mapenzi katika hobi hizo, basi tambua
kuwa huyo mrembo wako amekunywesha sumu ya penzi na sasa huwezi hata kuitumia
vema mantiki yako.
Mbaya zaidi, iwapo utabaini
kuwa marafiki zako wapya ni marafiki wa siku zote wa mpenzi wako na hobi zako
ni zile za mpenzi wako, basi tambua kuwa huna tena nafsi yako, bali
umejisalimisha mzima mzima kwa mpenzi wako.
Lakini msemo mmoja wa hekima
unatwambia usiweke mayai yako yote kwenye kikapu kimoja. Yamkini unaelewa.
7. KUKUBALI
KUPELEKESHWA.
Pengine unakumbuka kuwa kuna
nyakati ambapo ulikuwa na uwezo wa kujikita katika jambo moja na kulifanya kwa
umakini, huku ukiwa pia mwerevu, mjanja na unayejisimamia, lakini leo unayeyuka
kirahisi tu kama barafu iliyowekwa juani! Hii ni hatari kwa mustakabali wa
maisha yako.
Mbaya zaidi ni pale
utakapoiacha kazi yako inayokulipa vizuri na kufanya kazi nyingine kwa ajili ya
kumfurahisha mpenzi wako. Ukifika hali hii ujue wewe mwenyewe kuwa hapo hakuna
mwanamume.
8. UTAYARI
WA KUFA KWA AJILI YAKE.
Umewahi kujisikia kuwa na
utayari wa kufa kwa ajili ya mpenzi wako? Kama jibu ni “ndiyo”, basi fahamu kwa
hakika kuwa hayo uliyo nayo si mapenzi bali ni upumbavu. Pengine huku ndiko
kunywesha sumu ya mapenzi. Kwa hakika, hakuna mwanamke ambaye anastahili
kumfanya mwanamume yeyote kufa kwa ajili yake.
Yamkini wanaume wanaolengwa
katika makala haya si wavulana wanaosoma sekondari, waliobalehe majuzi, ambao
wakipenda au kupendwa hujiona kama wako katika sayari yao. Mwanamume
aliyepevuka hujiamini na hayaweki maisha yake yote mikononi mwa mwanamke, hata
kama mwanamke huyo angekuwa ndiye mrembo wa dunia.
Iwapo, ama kwa ujinga au kwa
kufahamu umewahi kumwambia mpenzi wako: “ukiniacha nitajiua,” na ukawa unaamini
hivyo kabisa, basi yamkini unahitaji kutafuta msaada wa ushauri nasaha, maana
kwa hakika umepotoka.
9. MUDA
WOTE UNAWASILIANA NAYE.
Vijana wa siku hizi ni
watumiaji wazuri sana wa simu, lakini iwapo utabaini kuwa asilimia kubwa ya
muda wako unautumia ama kwa kuongea au kuwasiliana kwa ujumbe mfupi na mpenzi
wako, basi fahamu kuwa kuna tatizo ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka.
Kumbuka kuwa mapenzi
hayachukui nafasi ya kila kitu. Yamkini huyo mpenzi wako amekukuta unaishi na
kuna mambo ya muhimu ya kufanya. Hebu achana na simu kwanza ufanye mambo ya
muhimu kuhusiana na maisha yako. Kama mpenzi wako hakwelewi katika hili basi
hakufai.
10. NDUGU
ZAKE WANAKUFUATILIA.
Iwapo utabaini kuwa
marafiki, ndugu na jamaa za mpenzi wako wanamtonya mpenzi wako kuhusiana na
kile wanachokiita mwenendo wako mbaya, usipuuze hali hii. Kuna uwezekano mkubwa
kuwa watu hawa wanayo sababu ya kuwa na wasiwasi na mwenendo wako, kwa hiyo
jichunguze na kuangalia jinsi unavyoenenda.
Hata hivyo, jambo hili si
ishara njema ya mustakabali mwema wa mahusianao yenu.
Iwapo mpenzi wako ataweka
watu wake wakufuatilie, maana yake halisi ni kwamba hakuamini. Katika hali kama
hii, haitarajiwi kuwa mustakabali wa uhusiano wenu utakuwa mzuri,
kwani kutakuwa na uingilizi mwingi wa ndugu, jamaa na marafiki
zake.
Unaweza kukubali kuendelea
kuishi katika hali hii kwa kisingizio cha mapenzi, lakini ukweli ni kwamba
hayatakuwa mapenzi bali karaha.
0 comments:
Post a Comment