`

Home » » WANANCHI WILAYANI TANDAHIMBA WAHIMIZWA KULIMA MAZAO YA CHAKULA

WANANCHI WILAYANI TANDAHIMBA WAHIMIZWA KULIMA MAZAO YA CHAKULA

Mtwara.
Wananchi wa wilaya ya Tandahimba mkoani mtwara, wamehimizwa kulima mazao ya chakula badala ya kutegemea zao la korosho ambalo ni la kibiashara kwani hata mazao hayo mengine yana soko la uhakika.


Wito huo umetolewa na mbunge wa Tandahimba Bw. Juma njwayo alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kijiji cha naputa, katika ziara yake ya siku saba kwaajili ya kuwatembelea wananchi wake ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara.

Njwayo amesema kuwa kwakuwa sasa mkoni humo imegundulika gesi asilia na wawekezaji wengi wamejitokeza kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda kutokana na kuwapo kwa umeme wa uhakika unaotokana na gesi na biashara nyingine idadi ya watu imeongezeka na mahitaji ya chakula ni makubwa ikilinganishwa na huko nyuma.

Amesema wilaya hiyo imebahatika kuwa na ardhi yenye uwezo wa kustawi kila aina ya mazao kama vile muhogo, alizeti, mahindi, jamii ya kunde na mazao mengine ambayo yanaweza kupata soko badala ya kuegemea kwenye korosho peke yake ambayo pindi inaposhuka bei wananchi hushindwa kujiendesha kiuchumi.

Aidha mbunge huyo amewahimiza wakazi wa vijiji vyote wilayani humo kujiweka tayari kuupokea umeme kwakuwa tathmini imeshafanyika na vijiji 50 kati ya 157 vinatarajia kupata umeme katika mwaka wa fedha unaokuja, na kusema kwamba wale watakaokutwa wapo tayari watakuwa wa kwanza kunufaika.

Njwayo Amesema wananchi wanatakiwa kujiwekea bajeti ya kifedha itakayowawezesha kugharamia zoezi la uunganishaji umeme majumbani, ikiwa ni pamoja na kuziandaa nyumba zao kwa kuziezeka kwa mabati badala ya nyasi kama ilivyo hivi sasa.

Mwisho..

0 comments:

Post a Comment

 
Designed By | Wishes co |
Copyright © 2014. Jicho La Mdadisi - All Rights Reserved
Template Modify by
Proudly powered by Wishes INK