Na mwandishi wetu.
Nanyumbu.
WAZAZI wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara imeelezwa kuchoshwa mechoshwa na hali ya elimu wilayani humo
kutokana na kushika nafasi ya mwisho kila mwaka na kuamua kuanzisha mikutano na
wazazi kila kata kutoa hamasa na kuwaelimisha ili kuinua kiwango cha elimu ambacho kwa sasa
ni janga kubwa ndani ya wilaya hiyo.
Akizungumza na wazazi,
viongozi na walimu katika mkutano huo, Mkuu wa wilaya hiyo Festo Kiswaga
alisema kuwa ili wilaya hiyo isonge mbele na kushika nafasi za juu kimkoa na
kitaifa lazima wazazi, viongozi na walimu washirikiane na kutimiza wajibu wao.
"Kwa siku ya leo
napenda tushirikiane changamoto inayohusu moja kwa moja jamii kuwa na mtazamo
hasi juu ya elimu na kutoipatia kipaumbele, hii ni changamoto kubwa na ambayo
ndio msingi wa changamoto nyingine,"alisema Kiswaga.
Alisema kuwa ndani ya
changamoto hiyo kuna mambo mengine ambayo ni pamoja na wazazi kutohimiza watoto
wao kuhudhuria shuleni ipasavyo, kutohudhuria vikao vya shule ili kujadili
masuala yahusuyo shule.
Aliongeza kuwa wazazi pia
kuwaamuru watoto wasifanye vizuri katika mitihani ya darasa la saba ili wasichaguliwe
kuendelea na masomo ya sekondari ili wasibugudhiwe tena na serikali kuwataka
kuwasomesha.
"Mambo haya ni madogo
yanapotamkwa lakini shughuli za maendeleo ni kubwa kwa kuwa athari zake ni
mbaya na za muda mrefu kusanyiko hili ni kujaribu kufufua hamasa ya wananchi katika
kushiriki kwenye shughuli za elimu kwa hali na mali,"alisema.
Naye Afisa Elimu wa Wilaya
hiyo, Angelina Makwaya alisema kuwa mikutano hiyo itafanywa kila kata ili kuwapatia
elimu wazazi ili wajue umuhimu wa elimu kwa watoto wao ili kujenga taifa la
wasomi.
"Kikubwa sisi kama
wenye dhamana ya kusimamia elimu tumechoshwa na kuwa wa mwisho kielimu kimkoa
na kitaifa hiyo hamasa hii itatufanya tuamshe elimu na kufanya vizuri kila kwa
ngazi zote,"alisema Makwaya.
Alisema kuwa wazazi wa
wilaya hiyo hawana muamko wa elimu ambapo wanaona ni kawaida kwa mtoto kwenda disko
na video usiku bila kujua shuleni amefanya nini na maendeleo yake yapoje kitu kinachokwamisha sekta ya elimu.
Mmoja wa wazazi
waliohudhuria mkutano huo, Augustino Mapunda alisema kuwa suala la wazazi
kutojua umuhimu wa elimu kwa watoto wao ni changamoto ambayo inazidisha vijana
wengi wasiojua kusoma na kuandika.
"Ukizunguka ndani ya
wilaya hii utakutana na vijana wengi vijiweni wakicheza Pool table na madereva pikipiki hawajui kusoma wala kuandika
sijui wazazi wenzangu wanafikiria nini kwa watoto wao hili ni janga kubwa kwa
wilaya yetu,"alisema Mapunda.
Wilaya ya Nanyumbu tangu
imeanzishwa mwaka 2006 ikitokea wilaya ya Masasi bado inafanya vibaya katika elimu
ya msingi na sekondari hali inayotishishia ustawi wa elimu wilayani humo na
kuendelea kuzalisha vijana wasiokuwa na ajira ambao wanabaki kukaa vijiweni na
kuilaumu serikali baada ya kuwalaumu wazazi wao.
MWISHO……………..
0 comments:
Post a Comment