Klabu ya soka ya YANGA
SC leo imepunguza pengo la pointi inazozidiwa na vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara Azam FC hadi kubaki pointi moja, kufuatia kuibwaga Kagera Sugar
ya Bukoba mabao 2-1 jioni hii katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo inayofundishwa na babu Mholanzi, Hans van der Pluijm kutimiza pointi 52, baada ya kucheza mechi 24, wakati Azam FC iliyocheza mechi 23 ina pointi 53 kileleni.
Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya tatu, akiunganisha krosi maridadi ya Mrisho Ngassa.
Didier
Kavumbangu aliifungia Yanga SC bao la pili dakika 36 akimlamba chenga
kipa Agatony Anthony baada ya kupokea krosi nzuri ya Simon Msuva na
kuituliza kifuani kwanza, kabla ya kumtesa kipawa timu ya Bukoba.
Sifa zimuendee Mrisho Ngassa kwa bao hilo, kwani ndiye aliyeanzisha shambulizi hilo kwa kuwatoka wachezaji wa Kagera na kumchomekea Simon Msuva mpira kwenye njia akapiga krosi.
Hilo lilikuwa bao la 30 katika mashindano yote kwa Kavumbangu ndani ya mechi 60 alizoichezea Yanga SC katika misimu miwili. Msuva naye amecheza mechi ya 30 leo akijivunia kutoa krosi ya bao.
Beki Ernest Mwalupani alikuwa mwenye bahati kwa kuonyeshwa kadi ya njano dakika ya 64 na refa Maalim Abbas wa Rukwa akimtuhumu kuwapendelea wenyeji katika kosa ambalo lilistahili kadi nekundu.
Daudi Jumanne aliifungia Kegara Sugar bao la kufutia machozi dakika ya 62 kwa shuti kali.
Wakati huo huo huko Mlandizi, mkoani Pwani mchezo kati ya wenyeji Ruvu Shooting na Azam FC ya Dar es Salaam uliokuwa ufanyike jioni ya leo Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani umeahirishwa hadi kesho kufuatia mvua kubwa.
Timu hazikuwahi hata kuingia uwanjani kupasha misuli moto kutokana na mvua kubwa na Uwanja kujaa maji na ilipowadia Saa 10:20 waamuzi wa mechi hiyo waliingia uwanjani kukagua na kuvunja mchezo.
Kilifuatia kikao cha pande zote nne, baina ya viongozi wa Ruvu na Azam pamoja na TFF na marefa ambao waliafikiana mechi ichezwe kesho iwapo hali itakuwa nzuri.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alikuwepo na kushuhudia hali hiyo.
Isihaka Shirikisiho wa Tanga ndiye aliyetarajiwa kuwa refa wa mchezo wa leo, akisaidiwa na Hassan Zani na Agness Pantaleo wote wa Arusha na refa wa akiba mwenyeji, Simon Mbelwa.
Azam yenye pointi 53 itaendelea kuishi kileleni mwa Ligi hata Yanga SC inayocheza na Kagera Sugar hivi sasa mjini Dar es Salaam itashinda, kwani wana Jangwani hao watatimiza pointi 52 huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
0 comments:
Post a Comment