WATU 26 wamekufa na wengine 26
kujeruhiwa katika ajali mbili tofauti za barabarani zilizotokea jana,
Singida na Lindi. Ajali ya kwanza iliyoua watu 13 papo hapo na mmoja
kujeruhiwa, ilitokea jana asubuhi, baada ya gari dogo la abiria aina ya
Toyota Noah walilokuwa wakisafiria, kugongana uso kwa uso na lori la
mizigo eneo la Isuna, barabara kuu ya Singida-Dodoma.
Ya pili ni iliyoua watu 13 na kujeruhi
wengine 25 baada ya basi la Al Hamdullilah walilokuwa wakisafiria kutoka
Dar es Salaam kwenda Mtwara, kuacha njia na kupinduka mtaroni saa 7.30
mchana.
Waliokufa na kutambuliwa katika ajali ya
kwanza ni Haji Mohamed (29), mkazi wa Msisi, Singida; Salma Omar wa
Itigi, Manyoni; Mtunku Rashid (68), Swalehe Hamis (28), Nyamumwi Omari
(10) na Samir Shaban (20) wote wa Saranda, Manyoni.
Wengine ni Mwareki Nkuwi (35) wa Ikungi,
Athman Kalemba (38), Ramadhan Mkanga na Omar Shaban wa Saranda na
wengine watatu ambao hawakutambulika mara moja.
Majeruhi ambaye amelazwa katika chumba
cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya mkoa, jina lake pia
halijafahamika. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela,
alisema mjini hapa jana kuwa ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi
ikihusisha lori namba T 687 AXD aina ya Scania mali ya Mussa Transport
ya Dar es Salaam na Noah namba T730 BUX, mali ya Mbua Ndofo wa Ikungi,
Singida.
Alieleza kuwa Noah ilikuwa inatoka Itigi
kwenda Singida wakati lori likitoka Mwanza kwenda Dar es Salaam likiwa
na shehena ya samaki wabichi. Kwa mujibu wa Kamanda Kamwela, chanzo cha
ajali hiyo kinaweza kuwa ni uzembe na mwendo kasi na baada ya ajali
kutokea, dereva wa lori na utingo wake walikimbilia kusikojulikana.
Kuhusu ajali ya pili, Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, alithibitisha kutokea kwa vifo
hivyo na kuongeza kuwa basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Ali Hamza.
Akisimulia kuhusu ajali hiyo, abiria wa
basi hilo aliyepata majeraha mkononi, George Steven alidai kuwa chanzo
cha ajali hiyo ni mwendo kasi na mvua iliyokuwa inanyesha iliyosababisha
dereva asione vizuri mbele.
Kabla ya kupinduka, Steven alidai basi
hilo liliyumba na kuvamia mtaro na kupinduka na kuungwa mkono na abiria
mwingine Joseph Francis. Nako huko Mbeya ajali nyingine imehusisha
magari zaidi ya matano ambapo inadaiwa gari moja liligonga magari
mengine matano.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Parseko Kone,
kutokana na vifo hivyo.
“Nimeshitushwa, nimesikitishwa na
kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya watu 13 akiwamo mtoto wa miezi
minne vilivyotokea katika eneo la ajali, baada ya gari walilokuwa
wakisafiria kutoka Itigi kwenda Singida kugongana uso kwa uso na lori
eneo la Isuna,” alisema Rais Kikwete katika taarifa ya Ikulu iliyotumwa
jana.
Rais alisema inatia simanzi kuona ajali
zikiendelea kutokea na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia hususan
mtoto mdogo kama huyo wa miezi minne, kusababisha ulemavu wa kudumu kwa
baadhi ya watu na uharibifu wa mali kutokana na makosa ya binadamu
katika uendeshaji wa vyombo vya moto.
“Nawaomba wanafamilia wawe na moyo wa
uvumilivu, subira na ujasiri hivi sasa wanapougulia machungu ya
kupotelewa na ndugu zao,” alisema Rais Kikwete kwa masikitiko.
Aidha, Rais alimwomba Mwenyezi Mungu,
azipokee na kuzilaza mahali pema peponi roho za marehemu wote, na
aliwahakikishia wafiwa kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba huo
mkubwa. Vilevile alimtakia ahueni kijana majeruhi wa ajali hiyo aweze
kupona haraka na kurejea katika hali ya kawaida na kuungana tena na
ndugu na jamaa zake. Hizi ni ajali mbili kubwa za kwanza kutokea
barabarani na kuua watu wengi tangu kuanza kwa mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment