`

Home » » MADIWANI RORYA WATAKA USHURU UKUSANYWE KWA LAZIMA.

MADIWANI RORYA WATAKA USHURU UKUSANYWE KWA LAZIMA.

Na Mwandishi wetu.

TARIME.

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ambaye pia ni Diwani wa kata ya Roche  Charles Ochelle(CCM) amesema kuwa siasa isihusishwe kwenye suala la mapato nakwaba ushuru wa vibanda vilivyoko Shirati na Utegi lazima ukusanywe.

Ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani baada ya Madiwani kulalamika na kudai kuwa kushuka kwa mapato ya Halmashauri kunatokana na viongozi wa  CCM ambao ni Mwenyekiti wa CCM Samwel Keboye na Mbunge wa Jimbo  Lamec Airo Wilayani Rorya kuwagomesha wananchi  kutolipa ushuru wa vibanda kupitia kwenye mikutano yao ya hadhara.

Ochele alisema kuwa siasa haipaswi kuhusishwa kwenye masuwala ya maendeleo kwani Halmashauri inategemea  mapato yanayotokana na makusanyo ya ndani Wilayani humo na kwamba iwapo wanasiasa wataendelea kuwachochea wananchi kutolipa ushuru Halmashauri itashindwa kujiendesha.


Diwani wa kata ya Ikoma Laurent Adrian (CCM) alisema kuywa mapato ya Halmashauri  yameshuka kutoka milioni 57 hadi milioni 25 ambapo sababu kubwa  ni malumbano ya Viongozi wa Serikali na Viongozi wa siasa ambapo viongozi hao wa siasa  wamezuia ushuru wa pikipiki uliofutwa na halmashauri na wameendelea kuwazuia watu kulipa ushuru wa vibanda.

Diwani wa kata ya Mkoma  Lazaro kitoli (CHADEMA) alisema kuwawananchi wa Shirati wamekataa kulipa ushuru wa vibanda”mimi mwenyewe nilimsikia Mbunge kwa masikio yangu mbele ya mkutano wa hadhara Shirati nikiwa nimekaa na Diwani Pendo Odelle(ccm) akawazuia wananchi wasilipe ushuru wowote kwamadai kuwa wananchi wanatoa ushuru nawakati soko ni chafu”alisema.

Diwani wa kata ya Kigunga Magesa Magige(CCM) ambaye pia  niMwenyekiti wa kamati ya ya uchumi ujenzi na mazingira yeye aliwataka viongozi hao wa kisiasa juu ya wao kuwazuia wananchi wa Shirati na aUtegi kutolipa ushuru wa vibanda waitwe kwenye kamati ya maadili ili wajadiliwe.

Mwenyekiti Ochelle alitoa amri na kuiagiza halmashuri kutoa gari na kwenda kukusanya uchafu Shirati pia alisisitiza kuwa ushuru wa vibanda utaendelea kukusanywa hivyo akawataka wananchi kuendelea na ulipaji wa ushuru kwakuwa ndiyo tegemeo kwa maendeleo ya wana Rorya.

Hata hivyo Madiwani  walimtaka Mwenyekiti wa CCM Samwel Keboye na Mbunge Rameck Airo kwenda kwa wananchi kuwahamasisha kulipa ushuru wa vibanda kwani wao ndiyo waliowazuia wananchi na ndiyo wanapaswa kwenda kuwahimiza kwakuwa wao ni viongozi wakubwa wanasililizwa na wananchi na walisemalo wananchi wanalitekeleza.

Mwisho,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,

0 comments:

Post a Comment

 
Designed By | Wishes co |
Copyright © 2014. Jicho La Mdadisi - All Rights Reserved
Template Modify by
Proudly powered by Wishes INK